Ubongo ni sehemu ya ajabu sana katika mwili wa binadamu, haujulikani kama ni nyama nyeupe, ute mkavu wa yai ama ni kitu gani. Wataalamu wameshinda kuufananisha ubongo kwa kukosa picha halisi yenye kufanana na ubongo zaidi ya ubongo wenyewe. Ubongo ndio makao makuu ya fikra, mijadala yote ya fikra katika mwili wa binadamu hufanyika katika ubongo.
Njia kuu za kupevusha fikra kwa kuruhusu ubongo kufanya maamuzi chanya
Mazoezi ya mara kwa mara
Mazoezi yana uwezo wa kuchangamsha chembe hai za ubongo kwa kupitia mfumo wa neva “neurogenesis”. Pia mazoezi ya misuli husaidia katika kupunguza msongo wa mawazo, hii ni njia rahisi na ni bure.
Hii inawezekana kwa kucheza michezo inayotumia akili kama drafti na michezo mingine ambayo pia hupatikana katika simu kama “Sudoku, Crosswords puzzles” ambayo huchangamsha na kuuamsha ubongo.
Kusoma
Hii ni njia nzuri ya kusaidia kukuza uwezo wa kufikiri, watafiti wanasema unaposoma kitabu ambacho hukuwahi kusoma au magazeti na majarida inasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uwezo wa kufikiri na ndio maana wazazi wanashauriwa kuwahimiza watoto kupendelea kusoma ili kujifunza na kupanua uelewa wao. Lakini angalizo ni kwamba unaposoma mathalani kitabu ambacho ni kirahisi sana hakikusaidii chochote bali kukufurahisha tu.
Kujifunza vitu vipya
Watafiti wa mambo husema akili ya binadamu inapopata nafasi ya kujifunza kitu kipya huupa ubongo changamoto ya kufikiri, kuwaza na kuwazua na hii hufanya ubongo kuwa ‘active’, kutofikia mwisho kujifunza kitu husaidia katika kufikiri, hii ni pale inapochagizwa na kupitia andiko ambalo hukuwahi kusoma.
Fanya Tafakari ( Meditation)
‘Meditation’ ni kitendo cha kufundisha ubongo kukumbuka na kutafakari. Pia kufanya tafakari husaidia kuongeza uwezo wa damu kuzunguka vizuri katika ubongo. Fanya tafakari angalau dakika 30 kwa siku ila sio lazima iwe kwa mara moja inawezekana ukaigawanya kwa dakika kumi kumi mara tatu kwa siku. Ila unashauriwa pale unapoamka ndo ufanya tafakari.
Kula Vizuri
Kuwa makini katika ulaji wa chakula kuna baadhi ya vyakula ni kwa ajili ya kujaza tumbo “Junk food” ila mojawapo ya vyakula unavyohitajika kula ni pamoja na samaki angalau mara tatu kwa wiki, nyama, watafiti wanasema chai (kwa asubuhi) ni chakula cha ubongo, Vitamini B na E, parachichi na pia inashauriwa kepuka chakula cha mafuta mengi.




